top of page

Mwongozo wa Kujiandaa na Ibada ya Umrah

Utangulizi​

Awali ya yote, ninamshukuru Allaah A’zza wa Jall[1] kwa kuweza kunipa uwezo kuandika machache kuhusu Ibada ya Umra. Ibada ambayo ni Sunnah iliyokokotezwa (na baadhi ya maulamaa wamesema ni wajibu) kwa kila Muislamu mwenye uwezo.

Pia Rehma na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) pamoja na Masahaba zake, Taabiina na wote waliofuata uongofu kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وسلم).

Ndugu yangu katika Imani unayetarajia kuitekeleza Ibada muhimu ya Umra. Mwongozo ni kitu muhimu katika kila jambo. Kiongozi wa Umra, ambaye ni wajibu wetu kumfuata, ni Mtume Muhammad (صلى الله عليه وسلم).

Imebainika kutokana na uzoefu kwamba ni vigumu sana kwa kila mwenye kutaka kuitekeleza ibada ya Umra, kuweza kukumbuka kila kinachohitajiwa katika kuitekeleza amali hii, hivyo ukiwa na mwongozo, utaweza kukusaidia wakati utakapotekeleza ibada hii.

Ndugu yangu katika Imani, kitabu hiki ni kidogo tu na kimeandikwa kwa lugha nyepesi kumrahisishia mwenye kuitekeleza Ibada hii ya Umra kuifahamu kirahisi na kuweza kumpa mwongozo kila mwenye kutaka kutekeleza ibada hii na kumrahisishia wakati wa kuitekeleza.

Kimekusanya mambo mengi ya kimsingi ambayo yanahusiana Umra pamoja na kufanya ziara katika Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم), Madina.

Kitabu kimejitahidi kuleta ushahidi wa Qur’aan na Sunnah katika kuhakikisha kila jambo linalofanyika lina ushahidi kwa kadri ya Allaah A’zza wa Jall alivyotujaalia.

Mwongozo huu utumike kwa yule ambae anataka kuitekeleza ibada ya Umra pekee na si katika wakati wa msimu wa Hijja.[2]

Ninamuomba Allaah A’zza wa Jall aijaalie amali hii ndogo iwe ni kwa ajili ya kupata radhi zake na iwanufaishe watakaojaaliwa kukisoma, pia iwaongoze watakaojaaliwa kuzitekeleza ibada hizi, bi idhni Llaah, Ibada yao ya Umra iwe maqbuul (itakabaliwe) na dhambi zao ziwe maghfuur (zisamehewe) na Sa’iy zao ziwe Mashkuur (zenye kushukuriwa). Aamin.

 

[1] Mwenye nguvu na Mshindi

[2] Ama yule mwenye kutaka kuitekeleza ibada hii katika msimu wa Hijja akitafute kitabu chengine cha ‘Mwongozo wa kuzitekeleza Ibada za Hijja na Umra’

  • Facebook
  • Twitter
  • LinkedIn
  • Instagram

Aina za watu wanaokwenda kutekeleza Ibada ya Umra

 

Katika kujifunza umuhimu wa Umra, nguzo, wajibu, taratibu, makatazo yake na kadhalika, wanaotia nia kwenda kufanya ibada hii takriban wanaweza kuwa katika moja ya hali tatu zifuatazo.

 

Ya kwanza

 

Hawaoni umuhimu wowote wa kujifunza na kujielimisha kabla ya Safari. Kundi hili huenda kufanya Umra na mara nyingi hufuata mkumbo tu bila ya kuwa na uelewa wa mambo wanayoyafanya.

 

Kundi hili mara nyingi lengo lao huwa kupata lile jina la kujulikana kama yeye ni Mu’utamir, Mu’utamirah, au amekwishatekeleza Umra.

 

Ya Pili

 

Hujifunza vizuri na kujielimisha vyema mambo yote muhimu ya ibada hii na huwa makini mno katika kuyatekeleza matendo ya ibada mpaka kuvuka mpaka ima katika kuyatekeleza au kuingiwa na mashaka na majuto kwa kuyakosa baadhi ya mambo huku shetani akiwazaini akili zao hasa katika mambo ambayo Maulamaa wametofautiana na kujikuta katika kutafuta majibu kwa masuala mazito huku wakishughulishwa katika Ibada yao ya Umra katika hukumu ya baadhi ya mambo badala ya kujikita na kuitekeleza ibada yenyewe.

 

Ya Tatu

 

Wanaofanya matayarisho ya ibada yao vizuri na kwa makini kwani wamefahamu vyema kwamba Safari hii ni Safari adhimu, ni Safari ya aina yake.

 

Hujiandaa vyema na huhakikisha maandalizi yao yanakuwa yamekamilka katika kila nyanja na kila idara.

 

Hawa hujiandaa kwa miezi si kwa mawiki na Umra kwa kuweza kufahamu uzito na umuhimu wa ibada hii.

 

Kundi hili hutafuta madarsa kwenda kujifunza kuhusu Umra, hutafuta semina kwenda kushiriki na kufaidika na mafundisho ya Umra.

 

Hufanya mazoezi ya mambo yote muhimu watakayopaswa kuyafanya hata kabla ya Safari. Huuliza wenye elimu pale wasipopafahamu.

 

Kundi hili huwa hawaachi kitu katika maandalizi yao huhakikisha kila kitu katika Safari yao kimekamilika. Huwa tayari kiimani na kiitikadi hivyo utendaji wao wa Manaasik za Umra unakuwa tofauti na makundi mengine.Kundi hili ni lile ambalo asaa litaiingia katika wenye kukubaliwa Umrah zao bi idhni Llāhi na kupata fadhila za Umra.

Fadhila za Umra

 

1   Hufuta madhambi

 

عن ‏ ‏أبي هريرة رضي الله عنه ‏أن رسول الله ‏صلى الله عليه وسلم قال: ‏‏ العمرة إلى العمرة كفارة لما بينهما والحج المبرور ليس له جزاء إلا الجنة. (البخاري ومسلم)

Kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) amesema: Umra hadi Umra hufuta madhambi yaliyofanyika baina yake na Umra iliiyopita; Na Hajj Mabruur (i.e., Hijja iliyokubaliwa) haina malipo mengine isipokuwa Pepo.

2    Huondosha ufukara

 

عَنْ ‏ ‏عَبْدِ اللهِ ابن مسعود رضي الله عنه ‏قَالَ قَالَ رَسُولُ اللهِ ‏ ‏صَلى اللهُ عَليْهِ وَسَلمَ:‏ ‏: ‏ ‏تَابِعُوا بَيْنَ الْحَجِّ وَالْعُمْرَةِ فَإِنهُمَا يَنفِيَان الفقرَ وَالذنوبَ كمَا يَنفِي ‏ ‏الْكِيرُ ‏ ‏خَبَثَ ‏ ‏الحَدِيدِ وَالذهَبِ وَالفِضَّةِ، وَليْسَ لِلْحَجِّ المبْرُور ثَوَابٌ دُونَ الْجَنةِ. (النسائي والترمذي)

 

Kutoka kwa Abdullah Ibn Masoud (رضي الله عنه) amesema kwamba Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) amesema: Fuatanisheni baina ya Hijja na Umra kwani huondosha ufakiri na (hufuta) madhambi kama mhunzi anavyoondosha uchafu kwenye chuma (cha kawaida), cha dhahabu na cha fedha. Na Hajj Mabruur haina malipo mengine isipokuwa pepo.

 

3     Umra itakayofanyika Ramadhaan ina fadhila sawa na Hijja

 

عن ابْن عَبَّاسٍ رضي الله عنهما قال: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لِامْرَأَةٍ مِنْ الْأَنْصَارِ: مَا مَنَعَكِ أَنْ تَحُجِّي مَعَنَا ؟ قَالَتْ: لَمْ يَكُنْ لَنَا إِلَّا نَاضِحَانِ (بعيران)، فَحَجَّ أَبُو وَلَدِهَا وَابْنُهَا عَلَى نَاضِحٍ، وَتَرَكَ لَنَا نَاضِحًا نَنْضِحُ عَلَيْهِ (نسقي عليه) الأرض، قَالَ: فَإِذَا جَاءَ رَمَضَانُ فَاعْتَمِرِي، فَإِنَّ عُمْرَةً فِيهِ تَعْدِلُ حَجَّةً. (البخاري ومسلم

 

Kutoka kwa Ibn `Abbas (رضي الله عنهما) amesema: Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) alimwambia mwanamke kutoka kwa Ansaar: “Kitu gani kilichokuzuia usihiji na sisi?” Akasema: “Tuna Ngamia wawili tu. Baba watoto na mwanawe wamekwenda Hijja na wametumia Ngamia mmoja, na wamemwacha Ngamia mwengine ili tumtumie kwa ajili ya kuchota maji na kumwagilia (shambani)”. Mtume akasema: “Itakapowadia Ramadhan nenda katekeleze (Ibada ya) Umra kwani Umra hii ni sawa na Hijja”. Na katika riwaya ya Muslim: “… ni sawa na kuhiji pamoja na mimi.”

Vipi ujiandae kwa Safari ya Umra

 

Kila Ibada huhitaji maandalizi. Ndugu yangu katika Imani, uliyetia nia ya kutaka kufanya Safari hii, zingatia yafuatayo kwanza ili lengo la Ibada uliyoikusudia lifanikiwe kwa Tawfiyq ya Allaah A‘zza wa Jall

 

Jiandae kiimani

 

•Jielimishe nini maana Ikhlaas na uhakikishe unakuwa nayo. Lengo lako kukusudia kufanya Safari, In shaa Allaah, liwe ni kwa ajili ya Allaah A’zza wa Jall na kujaribu kuwa karibu na Ar Rahmaan. Ikiwa lengo ni kinyume cha hili basi badilisha lengo lako kwanza. Allaah A’zza wa Jall Anasema: •وَأَتِمُّواْ ٱلۡحَجَّ وَٱلۡعُمۡرَةَ لِلَّه•“ Na timizeni Hijja na Umra kwa ajili ya Allaah

 

•Tubu makosa yako uliyofanya kwa Allaah A’zza wa Jall toba iliyo ya kweli inayothibitisha na kuonesha majuto kutoka ndani ya moyo wako na kuazimia kutoyarudia tena makosa hayo.

 

 

•Jisalimishe nafsi yako na moyo wako kwa Allaah A’zza wa Jall kwani Safari ya Umra si ya kufanyiwa mzaha ni Safari ya kupewa heshima ya kipekee katika Safari zote katika maisha yako

 

•Thamini mwaliko na wito uliopata kutoka kwa Allaah A’zza wa Jall kuwa ni miongoni mwa wageni wake. Jitahidi na jiandae uwe miongoni mwa wageni bora wa Ar Rahmaan.

 

•Jitathmini nafsi yako mwenyewe na tambua mapungufu yako ya kiimani na uyarekebishe. Usifanye Safari ya Umra ilhali unajua ukirudi utaendelea kufanya maasi na madhambi, bali tia nia na kuazimia kutoyarudia huku ukiomba tawfiyq kutoka kwa Allaah A’zza wa Jall.

 

•Tumia fursa nzuri utakayoipata kuwa karibu Allaah A’zza wa Jall hasa pale utakapoona moyo wako umeingiwa na Imani, umeingiwa na unyenyekevu na kuwa karibu mno na Allaah A’zza wa Jall.

 

 

Jiandae kielimu na kifiqh

 

Unapokwenda Makkah unakwenda kufanya Ibada muhimu ya Umra. Hivyo inakuwajibikia kuifahamu vyema Ibada hii na taratibu zake.Hivyo:

 

•Jielimishe vizuri kuhusu ahkaam (hukumu) za Umra na uwe makini wakati ukizitekeleza.

 

•Jizoeshe kuzitekeleza amri zote katika dini hasa kusimamisha sala katika nyakati zake kwa kusali Jamaa misikitini, kusoma Qur’aan, kumkumbuka Allaah A’zza wa Jall na kadhalika.

 

•Jielimishe na kujifunza baadhi ya dua zilizomo katika Qur’aan na Sunnah na kuzihifadhi vizuri zitakusaidia sana.

 

•Jielimishe jinsi ya kuisali sala ya maiti pamoja na utaratibu wake utakutana nayo takriban katika kila sala katika Misikiti Mitakatifu ya Makkah na Madina.

 

•Jielimishe adabu za kuzuru makaburi na taratibu zake.

 

•Jielimishe jinsi ya kusali sala za Safari pamoja na hukumu zake za kuchanganya na kuzipunguza.

 

•Jielimishe jinsi ya kutayammam pamoja na kufuta kwa viatu au soksi ni vitu ambavyo utavitumia utakapokuwepo kwenye Umra hivyo vifahamu vizuri taratibu zake.

 

•Jifunze baadhi ya dua kutoka katika Qur’aan na Sunnah zilizothibiti

 

•Kuwa karibu na waliokuwa na elimu na usione aibu kuuliza hasa jambo usilolijua au kulifahamu vyema kwani makosa yanaweza kutokea.

 

•Sikiliza vizuri maelekezo ya viongozi wa kundi lako hasa wakati wa kutekeleza manaasik ya Umra.

 

Jiandae kimwili na kiafya

 

•Umra ni moja katika mitihani hivyo utakabiliwa na kwenda mwendo wa masaf marefu, joto kali, muda mrefu wa kusimama, muda mrefu wa kusubiri, muda mrefu kuwepo Msikitini, kusukumwa, kukanyagwa na kadhalika hivyo

 

•Fanya mazoezi ya kimwili ili kuuweka mwili sawa ima kwa kutembea au Jogging angalau mwezi mmoja kabla ya Safari.

 

•Hakikisha mazoezi utakayofanya hayatoweza kukupatia majeraha au maumivu ya muda mrefu.

 

•Kula vyakula vyenye rutuba nzuri kabla ya Safari na wakati upo Safarini hasa vya matunda.•Kunywa maji kwa wingi ili mwili uweze kukabiliana na hali ya joto pia uhakikishe una maji ya akiba.

 

•Hakikisha unatumia dawa mara tu ukijisikia kuumwa.

 

•Hakikisha umechukua dawa za mafua na kifua kwani kuna uwezekano mkubwa wa kuambukizwa maradhi haya kutokana na wingi na msongamano wa watu hivyo jiandae mapema.

 

•Jipange kutumia muda wako vizuri Makkah na Madina usijikalifishe mpaka ukajichosha kwa sehemu moja na kushindwa kufanya Ibada sehemu nyengine.

 

Jiwekee mazingira bora kabla ya Safari

 

Unapokwenda kutekeleza Ibada ya Umra kuna uwezekano wa kutorudi na kupata fadhila za kufariki katika miji mitakatifu, pia kuna uwezekano wa kurudi ukiwa umesamehewa madhambi yako yote hivyo kabla ya Safari hakikisha:

 

•Umeandika Wasia ambao utabainisha kile ambacho ni haki yako na kile ambacho ni haki ya wengine.

 

•Umerudisha amana yoyote ambayo iko mikononi mwako na kama haitowezekana basi kuomba idhini ya kuwa na amana hiyo.

 

•Umerudisha kila ulichokipata kwa njia isiyokuwa ya haki kwa wenyewe hata kiwe kidogo vipi ikiwezekana.

 

•Haikuwezekana, walipe uliowachukulia haki zao kwa mujibu wa thamani ya haki zao. Kama haiwezekani, basi ni lazima uwaombe msamaha kwa uliyowahi kuyafanya dhidi yao.

 

•Umeomba radhi kwa yeyote ambae umemkosea kwa kujua au kutokujua.

 

•Chumo utakalotumia kwa ajili ya Safari liwe limepatikana katika njia ya halali.

 

Jiandae kimkakati

 

Safari ya Umra ni Safari kwa ajili ya Ibada na si vyenginevyo. Ni Safari muhimu kwani ni njia mojawapo itakayotupeleka peponi kwa tawfiyq ya Allaah, A’zza wa Jall; hata hivyo ina changamoto zake pia hivyo:

 

•Jiwekee malengo yanayowezekana katika kutekeleza ibada kutokana na hali yako na uwezo wako.

 

•Kuwa na mpangilio maalum wa Ibada ambao utaufuatilia kwa karibu na kuhakikisha unakamilisha malengo, siku hadi siku na pia kuyapitia kwa kuyafanyia tathmini katika utekelezaji wake kila siku.Changamoto utakazokabiliana nazo

 

•Kuchelewa kwa usafiri au kusubiri muda mrefu kutoka sehemu moja kwenda nyengine.

 

•Msongamano mkubwa katika sehemu muhimu za Ibada na hivyo kushindwa kupata fursa ya kuwa karibu na sehemu hizo.

 

•Kupanguka kwa ratiba mliyopangiwa

 

•Usumbufu wa waumini wengine, kusukumwa,

Vituo vya kuhirimia (Mawaaqit)

 

 

Neno Mawaqit (مواقيت) ni wingi wa neno Miqaat (ميقات):

 

Ni mipaka au vituo viliyowekwa ambayo kwa anaetaka kuelekea Makkah kwa ajili ya Hijja au Umra atatakiwa ahakikishe amehirimia kwa Hijja, Umra au yote mawili kwenye vituo.

 

Ikiwa Muislamu anaekusudia kufanya Hijja au Umra atavuka mipaka ya Miqaat bila ya kuhirimia itambidi arudi tena kwenye kituo cha kuhirimia. Kama hakurudi itambidi achinje mnyama kama ni fidia.

 

عن ‏ ‏ابن عباس رضي الله عنه ‏قال إن الـــنــبي ‏صـــلى الله عـــــــلـيه وســــــلم ‏وقَّـــــتَ ‏لأهــــــل المــــــــديــــــنة ‏:‏ ‏ذا الحــــلـــــيــفــة ولأهـــــــل الـشـــــــام الجــــحــفــة ولأهـــــــل نــجـــــــد قـــــــرن المــــــنـــازل ولأهــــــل الــــيـمــن يـــلـــمـــلـــم، هُــــنَّ لَهُــــنَّ ولـــمـن أتـــى عـــلـــيــهـــن مـــــن غـــــيرهــن مـــمـــــن أراد الحــــــج والـــــعـــمــرة، ومـــــن كــــــان دون ذلك فــــمــن حـــيــث أنــــشـأ، حتى أهــــــلُ مـــــكــةَ مـــــــــن مـــــــكــة. ( البخاري ومسلم )

 

 

‏Kutoka kwa Ibn Abbas (رضي الله عنه): Mtume (صلى الله عليه وسلم) amepaweka Dhu-l Hulayfah kama ni ni kituo cha watu wa Madina; Al-Juhfa kwa watu wa Sham; Qarn al-Manazil kwa watu wa Najd; na Yalamlam kwa watu wa Yemen; na vituo hivi pia kwa watu waliopo hapo, na wale watakaopitia vituo hivi kwa ajili ya kutekeleza Hijja na Umra na kwa wanaokaa ndani ya mipaka ya vituo hivi atahirimia pale atakapoanzia na watu wa Makkah watahirimia wakiwa Makkah.

 

 

عن أبي الزبير عن جابر رضي الله عنه قال: سمعت، أحسبه رفع الحديث إلى رسول الله صلى الله عليه وسلم، قال: مهل أهل المدينة من ذي الحليفة، والطريق الآخر الجحفة، ومهل أهل العراق من ذات عرق، ومهل أهل نجد من قرن، ومهل أهل اليمن من يلملم. ( مسلم )

 

Abu Zubair alimsikia Jabir ibn 'Abdullah (رضي الله عنه) akisema: Nilimsikia (na nadhani alichukua moja kwa moja kutoka kwa Mjumbe wa Allah) akisema: Kwa watu wa Madina, Dhu-l Hulayfah ndiyo kituo chao cha kuhirimia na kwa wanaopitia njia nyengine (kama Syria) kituo chao ni Al Juhfah; na kwa watu wa Iraq ni Dhatu 'Irq; na kwa watu wa Najd ni Qarn (al-Manazil) na kwa watu wa Yemen ni Yalamlam .

Kuhirimia kwa ajili ya Umra

 

Makkah kwanza

 

•Ikiwa Makkah ndiyo kituo chako cha kwanza kwenye Safari yako itakubidi uhirimie kabla ya ndege kutua Jeddah. Jeddah ipo ndani ya vituo vya kuhirimia.

 

•Tia nia ya kuhirimia na kuanza kusoma Talbiyah wakati mtakapotangaziwa mkiwa ndani ya ndege na kabla ya kutua Jeddah, takriban:

 

•Dakika 20 kwa ndege zinazotokea Ulaya, Jordan, Syria n.k (kupitia kituo cha Rabigh)

 

•Dakika 30 (kupitia kituo cha Qarn al-Manazil) – kwa ndege zinazotokea falme za Kiarabu, Oman n.k.

 

•Utahitaji kuwa na mashuka ya Ihraam kwa ajili ya Umra kabla ya Safari. Unaweza kununua mengine Makkah au Madina au kuosha Ihraam uliyonayo.

 

•Hakikisha mashuka ya Ihraam umeyaweka kwenye mkoba wako wa mkononi.

 

•Vaa Ihraam yako kwenye kituo cha mwisho (Transit) kabla ya kuelekea Jeddah kwani huwa vigumu kuivaa Ihraam ukiwa ndani ya ndege

 

Madina kwanza

 

•Ikiwa kituo chako cha kwanza ni Madina hutokuwa na haja ya kuhirimia au kuvaa Ihraam.

 

•Utaweza kununua mashuka ya Ihraam Madina.

 

•Kituo chako cha kuhirimia Umra kitakuwa Dhu-l Hulayfah (ambacho pia hujulikana kama Abyar 'Ali).

Maandalizi ya Ihraam

 

Wanaume

 

• Punguza sharubu

 

• Kata kucha za vidole vya mikono na miguu

 

• Jisafishe sehemu za siri kwa kunyoa pamoja na kwapani

 

• Koga josho maalum kwa ajili ya kuhirimia. Ni Sunnah

 

• Jipake manukato mwilini (kichwani na kwenye ndevu…)

 

• Vaa Ihraam yako (Rida’ & Izar – mashuka mawili meupe) (رداء و إزار)

 

• Sali rakaa mbili za Sunnah, au sala yoyote iliyoingia katika wakati wake

 

 

Wanawake

 

• Kata kucha za vidole vya mikono na miguu

 

• Jisafishe sehemu za siri kwa kunyoa pamoja na kwapani

 

• Koga josho maalum kwa ajili ya kuhirimia. Ni Sunnah

 

• Vaa nguo zako za kawaida

 

• Usifunike uso na viganja

 

• Sali rakaa mbili za Sunnah, au sala yoyote iliyoingia katika wakati wake

 

• Mwanamke alie kwenye siku zake za hedhi au nifasi atakoga na kuhirimia lakini hatosali Rakaa mbili za Ihraam.

 

 

Angalizo:

 

Mpaka muda huu, uliyoyafanya yote ni maandalizi kwa ajili ya Ihraam na si kuhirimia kwenyewe. Maandalizi haya yanaweza kufanyika nyumbani au sehemu uliyofikia (Hoteli).

 

Utakapofika kwenye kituo (cha kuhirimia) na baada ya kusali (rakaa mbili) ndiyo utatia nia na kusema:

 

Labbayka Allahumma Umratan

 

Nimekuitikia Ewe Mola, (nimenuilia) Umra

 

Kuanzia hapa sasa tayari upo katika hali ya Ihraam!Baada ya kutia nia utaanza kusoma Talbiyah kwa sauti kubwa:

 

لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ، لَبَّيْكَ لاَ شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ، إِنَّ الْحَمْدَ، وَالنِّعْمَةَ، لَكَ وَالْمُلْكَ، لاَ شَرِيكَ لَكَ

 

Labbayka -Llaahumma labbayk labbayka laa shariyka laka labbayk inna-l hamda wa-n ni'mata laka wa-l mulk, laa shariyka laka

 

Tumeitikia Ewe Mola tumeitikia, Tumeitikia kwani huna Mshirika Tumeitikia, Hakika Himdi (shukurani) na Neema zote ni zako na Ufalme ni wako na huna mshirika.

 

Talbiyah iendelezwe kusomwa (si lazima muda wote lakini ni vyema mara nyingi) mpaka utakapoiona Al Ka’abah.

 

Isome Talbiyah:

 

•Wakati wa kupanda au kushuka utakapokuwa Safarini,

 

•Utakapojiunga na kundi la watu,

 

•Kila baada ya Sala,

 

•Kila asubuhi na jioni

 

Maulamaa wengi wamependekeza kwamba mwanamke atasoma Talbiyah kwa sauti ya chini. Hata hivyo Sh Albani anasema hakuna tofauti kati ya mwanamke na mwanamme kusoma Talbiyah kwa sauti kubwa isipokuwa tu kama atachelea Fitna.

 

Aaishah (رضي الله عنها) alikuwa akisoma Talbiyah kwa sauti kubwa.

 

Fadhila za Talbiyah

 

عن سهل بن سعد رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ما من مسلم يُلبِّي إلا لبَّى مَن عَن يمينه وشماله مِن حجر أو شجر أو مَدَر حتى تنقطع الأرضُ مِن هاهُنا وهاهُنا. (ابن ماجة والبيهقي والترمذي، والحاكم وصححه).

 

Sahl Ibn Sa’d amesimulia kwamba Mtume (صلى الله عليه وسلم) amesema: “Muislamu yeyote atakaeisoma Talbiyah chochote kilichopo upande wake wa kulia na kushoto miongoni mwa mawe, majabali, vichuguu pia vitasoma pamoja naye hadi masafa kadha wa kadha (mashariki na magharibi).

Mambo aliyohadharishwa (yaliyoharamu) kwa aliyehirimia Umra

 

Ukishahirimia kwa ajili ya Umra, kuna mambo ambayo umehadharishwa nayo na hutakiwi kuyafanya wakati upo katika hali ya Ihraam. Nayo ni:

 

1   Kuondoa aina yoyote ya nywele katika mwili kwa kunyoa, kukata au kunyofoa.

 

2   Kukata kucha ikiwa kwa kiwembe au hata kwa mkono au meno kwa kuzitafuna.

 

3   Kuvaa kofia, kilemba, kitambaa kwa mwanamme na kusitiri kichwa kwa kukusudia.

 

4   Kusitiri uso kwa kuvaa niqaab kwa mwanamke au kuvaa glovu kwenye mikono yake.

 

5   Kuvaa nguo zilizoshonwa na zenye kuchukuwa umbo la kiungo kwa kukusudia na kusitiri iwe mwili wote au sehemu ya mwili.

 

6   Kujitia manukato mwilini, kwenye Ihraam au kwenye nguo.

 

7  Kuposa, kufunga ndoa au kumfungia ndoa mtu mwengine.

 

8  Kufanya tendo la ndoa au kukumbatia mke/mume kwa matamanio.

 

9  Kuwinda na kuua mnyama.

 

10  Kwa mwanamme kuvaa viatu vya kutumbukiza kama buti, raba na kadhalika.

 

Tanbihi

 

Iwapo aliyehirimia amefanya yaliyohadharishwa kwa kutokujua, hatolazimika kutoa fidia yoyote.

 

Mambo aliyoruhusiwa kwa aliyehirimia Umra

 

1  Kuvaa pete au saa.

 

2  Kuvaa miwani.

 

3  Kuvaa mkanda au mkaja kuzuia Ihraam (isivuke).

 

4  Kuoga au kuisafisha Ihraam kwa kutumia sabuni isiyo na manukato.

 

5  Kubadilisha Ihraam ikiwa imechafuka.

 

6  Kujipaka mafuta yasiyokuwa na manukato mwilini.

 

7  Kwa mwanamme kuvaa viatu visivyokuwa vya kutumbukiza kama kandambili, malapa nk.

 

8  Kupiga chuku na kufanya Hijaamah

Aina za Fidia kwa kukiuka misingi na makatazo kwa aliyehirimia

 

Zimegawika katika makundi matatu

 

1    Kosa limefanyika kwa maksudi

 

Endapo aliyehirimia amefanya kosa ambalo anafahamu ni miongoni mwa mambo yaliyokatazwa, atawajibika kutoa fidia.

 

2    Kosa limefanyika kwa sababu ya dharura iliyojitokeza.

 

Endapo aliyehirimia amefanya kosa kwa sababu ya dharura kama kuwepo baridi kali na kuvaa sweta ili apate joto nae pia atawajibika kutoa fidia.

 

3    Kosa limefanyika bila ya kukusudia kwa kutokujua au kughafilika.

 

Endapo aliyehirimia amefanya kosa bila ya kukusudia, kwa kutokujua au kughafilika hatowajibika kutoa fidia.

 

Allaah A’zza wa Jall Amesema katika Qur’aan:

 

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذۡنَآ إِن نَّسِينَآ أَوۡ أَخۡطَأۡنَا‌ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحۡمِلۡ عَلَيۡنَآ إِصۡرً۬ا كَمَا حَمَلۡتَهُ ۥ عَلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِنَا‌ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلۡنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِۦ‌ۖ وَٱعۡفُ عَنَّا وَٱغۡفِرۡ لَنَا وَٱرۡحَمۡنَآ‌ۚ أَنتَ مَوۡلَٮٰنَا فَٱنصُرۡنَا عَلَى ٱلۡقَوۡمِ ٱلۡڪَـٰفِرِينَ

 

Mola wetu! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu! Usitubebeshe mzigo kama uliowabebesha wale walio kuwa kabla yetu. Mola wetu Usitutwike tusiyoyaweza, na utusamehe, na utughufirie, na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya makafiri.

 

Makosa yenye kuwajibisha Fidia kutolewa

 

1   Kuvaa nguo zilizokatazwa wakati wa Ihraam.

 

2   Kutumia manukato katika mwili au nguo.

 

3   Kukata kucha.

 

4   Kupaka mafuta yenye manukato.

 

5   Kufunika kichwa kwa mwanamme.

 

6   Kukata nywele.

 

7  Kuvaa soksi au glovu.

 

8   Kusitiri uso kwa mwanamke.

 

9   Kuvaa viatu vya kutumbukiza kwa mwanamme.

 

Ikiwa aliyehirimia ametenda moja ya makosa yaliyotajwa hapo juu atawajibika

 

A   kuchinja mbuzi au

 

B   Kuwalisha maskini sita au

 

C   Kufunga siku tatu

 

Unaweza kuchagua mojawapo katika fidia hizi na kutekeleza yoyote utakayoiona ni muwafaka kwako.

Nini Umra?

 

Katika lugha ya kiarabu Umra ni ziara.

 

Kisheria ni kufanya ziara katika nyumba kongwe kwa ibada (Al Ka’abah) kwa lengo makhsus na kujumuisha (katika ziara hii) Ihraam, Tawāf, Sa’iy, kunyoa au kupunguza nywele.

 

Ibada ya Umra inaweza kufanyika wakati wowote wa mwaka ila kwa wenye kwenda kufanya Ibada ya Hijja hutumia fursa hii pia kufanya ibada ya Umra.

 

Nguzo za Umra

 

Ni tatu

 

1   Kuhirimia

 

2   Kufanya Tawāf

 

3   Kufanya Sa’iy

 

Yaliyo wajibu kwa mwenye kufanya Umra

 

1   Kuhirimia katika Miqaat

 

2   Kunyoa au kupunguza nywele

 

Tanbihi

 

Ikiwa mwenye kuitekeleza Ibada ya Umra ataacha moja katika nguzo za Umra, Umra yake itakuwa haijakamilika na itambidi aifanye tena ibada hii.Ikiwa ataacha moja katika yaliyo wajibu kwa mwenye kufanya Umra itambidi alipe fidia kwa kuchinja mnyama na Umra yake itakubalika.

 

 

Namna ya kuitekeleza Ibada ya Umra

 

Ukifika mji wa Makkah, utakuwa tayari katika hali ya Ihraam, utakuwa tayari unaileta Talbiyah uliyoanza baada ya kuhirimia kwenye vituo vya kuhirimia.

 

Ni vizuri kupumzika kidogo mtakapofikia kuondosha machovu ya Safari kabla ya kuianza Ibada ya Umra ikiwezekana kwani ndivyo alivyofanya Mtume (صلى الله عليه وسلم).

 

Ni vizuri kukoga ikiwezekana kwani Abdullah ibn U’mar, (رضي الله عنهما) alikuwa akihakikisha kila akiingia Makkah hupitia Dhu Tuwa ambapo hulala usiku na asubuhi yake hukoga kama alivyokuwa akifanya Mtume (صلى الله عليه وسلم).

 

Hakikisha utakapokwenda Msikitini upo katika hali ya tohara na una Udhu.

 

Utakapofika Masjid al Haraam ni Sunnah kuingia kwa mguu wa kulia na kusema:

 

أَعُوذُ بِاللَّهِ الْعَظِيمِ وَبِوَجْهِهِ الْكَرِيمِ وَسُلْطَانِهِ الْقَدِيمِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ بِسْـمِ الله، وَالصَّلاةُ وَالسَّلامُ عَلى رَسولِ الله، اللّهُـمَّ افْتَـحْ لي أَبْوابَ رَحْمَتـِك

 

Auudhu Billaahil a’dhiym wabiwajhihil kariym wasultwaanihil qadiym mina shaytwaani rrajiym, BismiLlaah, Wasswalaatu Wassalaamu a’la Rasuuli Llaah, Allaahumma ftah liy abwaaba rahamtika

 

(Ninajilinda kwa Allaah Aliye mtukufu, na kwa Uso wake uli karimu, na Usultani wake wa zamani kutokana na shetani alierujumiwa. Ninaanza kwa jina la Allaah, na rehma na Amani zimfikie mjumbe wa Allaah, Ewe Mola nifungulie milango ya rehema zako)

 

Ukishaingia Msikitini na kuiona al Ka’abah, utakoma kusoma Talbiyah ndiyo mwisho wake kwa Umra na kabla ya kuanza Tawāf. Tawāf hii inaitwa Tawāful Umra.

 

Kabla ya kuanza Tawāf, kwa wanaume, ni Sunnah kuweka bega la kulia wazi (Idhtibaai)

 

Pia ni Sunnah kwa wanaume kwenda mwendo wa haraka (Jogging) na kikakamavu na kuweka kifua mbele katika mizunguko mitatu ya kwanza tu (Ar Ramal) ikiwezekana kama hakuna msongamano.

 

Kufanya Tawāful UmraTawāf ni ibada unayotakiwa uizunguke Al Ka’abah mara saba ukianzia sehemu lilipo jiwe jeusi (Hajar al as-wad) au usawa wake.Tawāf hii inaitwa Tawāful Umra ni moja katika nguzo za Umra hivyo lazima ifanyike vyenginevyo Umra haitosihi.

 

 

Masharti ya kusihi Tawāf

 

•   Hakikisha upo katika hali ya tohara kutokana na najsi na hadath na una Udhu.

 

•   Hakikisha unaanzia na kumalizia kwenye Hajar al as-wad.

 

•   Hakikisha umestiri utupu.

 

•   Hakikisha umekamilisha mizunguko saba.

 

•   Hakikisha Al Ka’abah itakuwa upande wako wa kushoto wakati wa kufanya Tawāf.

 

Namna ya kufanya Tawāf

 

•    Utaanza kwa kusema Bismillaahi Wallaahu Akbar au Allaahu Akbar huku ukilielekea Hajar al as-wad au ikiwezekana kama umelifikia Hajar al as-wad utaratibu ni kuligusa kwa mkono mmoja, kulibusu, kufanya sijdah juu yake na kisha ndio useme Allaahu Akbar

 

•    Baada ya kulibusu au kuashiria geuka kulia na Al Ka’abah iwe mkono wako wa kushoto.

 

•    Anza kuzunguka na mzunguko mmoja humalizika baada ya kufika Hajar al as-wad.

 

•    Ukifika Rukn al Yamani (nguzo ya tatu na kabla ya Hajar al as-wad) kama utaweza kuigusa basi iguse kwa mkono wa kulia na kisha useme Bismillaahi Wallaahu Akbar

 

•     Haikuwezekana kuigusa, usiiashirie na wala usisome Allaahu Akbar, endelea na Tawāf kama kawaida.•Baina ya nguzo ya Rukn al Yamani na Hajar al as-wad, imesuniwa kusoma:

 

•رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ

Rabbanaa Aatinaa Fiddunyaa hasanatan wafil aakkhirati hasanatan waqinaa a’dhaaba nnaar.

 

Kila ukipita hapo.

 

•   Wakati ukizunguka, unaweza kuomba duā za aina yoyote kwani hakuna duā maalum kwa ajili ya Tawāf hivyo omba duā utakazo kwa lugha yoyote, soma Qur’aan mtaje kwa sana Allaah A’zza wa Jall.

 

•   Ukimaliza mizunguko mitatu ya kwanza uliyofanya ar Ramal, utafanya Tawāf kwa mwendo wa kawaida kwa mizunguko mine iliyobakia.

 

•   Kila ukimaliza mzunguko na kuanza mwengine weka hesabu yako vizuri na hakikisha unasema Allaahu Akbar wakati wa kuanza mzunguko mwengine ukifika Hajar al as-wad .

 

•   Hakikisha umekamilisha Tawāf kwa kuzunguka Al Ka’abah mara saba. Baadhi ya makosa yanayofanyika wakati wa kufanya Tawāf

 

•   Kusali rakaa mbili unapoingia Masjid al Haraam.

 

•   Kutia nia ya Tawāf na kusema kwa sauti.

 

•   Kufanya Tawāf huku ukienda kwa haraka Tawāf tatu za mwanzo.

 

•   Kusukumana kwa ajili ya kulifikia Hajar al as-wad ili kulibusu

 

•   Kufanya Tawāf ilhali umeifunga mikono kama unasali.

 

•   Kufanya Tawāf bila ya kuwa na Udhu.

 

•   Kuzungumza na simu wakati upo katika Tawāf.

 

•   Kuzungumza mazungumzo yasiyokuwa na faida wakati wa Tawāf.

 

•   Kuongeza maneno katika duā zilizothibiti kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وسلم).

 

•   Kuashiria na kisha kubusu mikono au kufuta uso wakati wa kuanza Tawāf .

 

•   Kufuta kuta za Al Ka’abah ukidhani ni kupata baraka.

 

•   Kusoma Talbiyah wakati wa kufanya Tawāf Kidokezo

 

•   Unapofanya Tawāf jihisi kama unasali hivyo ule unyenyekevu unaopata kwenye sala ndio uupate kwenye Tawāf utakusaidia.

 

•   Jaribu kutumia dua tofauti katika dua zilizothibiti kila ukimaliza mzunguko na kuanza mzunguko mwengine.

 

•   Ukiwa hutaki zahma na msongamano, fanya Tawāf juu ghorofa ya kwanza au ya pili.

 

•  Ukiwa hutaki zahma na msongamano fanya Tawāf wakati usiku mkubwa au asubuhi baada ya alfajiri ambapo kunakuwa na unafuu kidogo.

 

•   Endapo wakati unaendelea kufanya Tawāf imesadifu kuingia wakati wa Sala ya fardhi na imekimiwa wakati hujakamilisha Tawāf; utasita hapo ulipo na kuunganika na waislamu kusali jamaa na baada ya sala kukamilika utaendelea na Tawāf bila ya kuanza upya.

 

Tahadhari kwa akinamama

 

Tawāful Umra ni ibada hivyo ni lazima uwe tohara na uwe na udhu wakati wa kuitekeleza.

 

Hivyo mwanamke aliye kwenye siku zake haruhusiwi kufanya Tawāf kwa sababu hayupo Tohara kisheria.

Kusali nyuma ya Maqaam Ibraahim

 

•    Baada ya kumaliza Tawāf, utaelekea nyuma ya Maqaam Ibraahim (sehemu aliyokuwa akisimama Nabii Ibraahim, a’layhis salaam kwa ajili ya Ibada) huku ukisoma:

 

وَٱتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبۡرَٲهِـۧمَ مُصَلًّ۬ى‌ۖ

 

•    Wattakhidhuu min maqaami Ibraahima muswallaa (Na alipo kuwa akisimama Ibraahim pafanyeni pawe pa kusalia)

 

•    Ukipata nafasi nyuma ya Maqaam, Sali rakaa mbili ikiwezekana.

 

•    Ikishindikana kutokana na msongamano wa waumini, sali sehemu yoyote ile ndani ya Msikiti inakubalika.

 

•    Katika Rakaa ya kwanza, soma Suuratul Faatihah (Alhamdu) kisha Suuratul Kaafiruun (Qul yaa ayyuhal kaafiruun) na kwa rakaa ya pili utasoma Suuratul Faatihah kisha Suuratul Ikhlaas (Qul huwa Llaahu ahad).

 

•   Ukimaliza na kutoa salaam unaweza kuomba duā kwa muda mchache tu.Baadhi ya makosa yanayofanyika wakati wa kusali nyuma ya Maqaam Ibraahim

 

•   Kukamata na kufuta kwenye kuta za Maqaam Ibraahim baada ya sala kwa kudhani kuna baraka na kheri.

 

•    Kuandika vikaratasi vyenye maombi na shida na kuvitundika Maqaam Ibraahim.

 

•    Kulazimisha kusali nyuma ya Maqaam wakati wengine wakiendelea na Tawāf.

 

•    Kutumia muda mrefu kuomba duā nyuma ya Maqaam.

 

•    Kuendelea kuomba au kusali Sunnah wakati Sala ya Jamaa ya fardhi imeshakimiwa .

 

•    Kusali rakaa zaidi ya mbili nyuma ya Maqaam.

 

•    Kuirefusha sala kwa kusoma sura ndefu na vihamo virefu

Kunywa maji ya Zamzam

 

•       Baada ya kumaliza Tawāful Quduum na kusali nyuma ya Maqaam Ibraahim, inapendekezwa kunywa maji ya Zamzam kama alivyofanya Mtume (صلى الله عليه وسلم).

 

•      Pia unaweza kujirashiarashia kichwani kama alivyofanya Mtume (صلى الله عليه وسلم).

 

•     Wakati unapokunywa, unaweza kuomba duā hasa ya kuponya maradhi kwani kuna hadithi ya Mtume (صلى الله عليه وسلم) inayothibitisha hivyo.

 

•     Kila ukiwemo Masjid al Haraam pendelea kunywa maji ya Zamzam huku ukiomba kwa Allaah A’zza wa Jall.

 

Fadhila za maji ya Zamzam

 

قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: مــــــاء زمــــــزم لــــمــــا شُــــــرِب لــــــه ( أحمد وابن ماجة )

 

Mtume (صلى الله عليه وسلم) amesema: Maji ya Zamzam ni kwa jinsi ya yalivyonuiliwa (wakati wa kunywa).

 

وقال رسول الله صلى الله عليه وسلم مـــــــاء زمـــــــزم فــــيــــه طــــــعــــام مـــن الـــطُّــــــعْــــم وشــــفـــاء مـن الـسُّـــقم ( البخاري ومسلم )

 

Na Mtume (صلى الله عليه وسلم) amesema: “ Maji ya Zamzam ni chakula kutokana na vyakula na Shifaa (dawa) kutokana na maradhi”

Kufanya Sa’iy

 

Sa’iy ni kutembea (na kwenda matiti) kati ya Jabal Swafā na Jabal Marwah.

 

Milima hii imo pembeni ya Msikiti ambako kumetengenezwa eneo maalum la kufanya ibada hii.

 

Utatakiwa ufanye mzunguko ukianzia Jabal Swafā na kumalizia Jabal Marwah (huu ni mzunguko mmoja).

 

Tanbihi

 

•   Sa’iy ni mojawapo katika nguzo za Umra hivyo lazima ifanyike vyenginevyo Umra haitosihi.

 

•   Si lazima uwe katika hali ya tohara utakapofanya Sa’iy ingawa ni vizuri zaidi na hupendeza kama utakuwa na udhu

 

•   Kwa wasiojiweza kwa ugonjwa au wenye ulemavu wanaweza kutumia vigari wheelchair wakati wa kufanya Sa’iy

 

•   Kama kuna Mu’utamir ambae anamsaidia asiejiweza hatowajibika kwenda Matiti wakati akipita katika nguzo za kijani

 

•   Sa’iy ikianzwa itabidi imalizwe hivyo kukitokea jambo lolote la kukufanya usite kama kwenda haja au Sala kukimiwa. Utasita kufanya Sai’y na utaendelea baada ya kumaliza.

 

•   Endapo huna kumbukumbu ya hesabu ni Sa’iy ya ngapi uliyofanya chukua hesabu ya chini kama ni 5 au 6 ifanye ni ya 5.

 

•   Kuzungumza kunaruhusika wakati ukifanya ibada ya Sa’iy hata hivyo kwa kuwa upo kwenye ibada ni vyema kutojihusisha na mazungumzo.Matakwa ya kisheria wakati wa kufanya Sa’iy ili Sa’iy ikamilike

 

•    Uifanye mwenyewe yaani usimuwakilishe mtu. (Ikiwa huwezi unaweza kutumia wheelchair)•Uwe upo katika hali ya Ihraam iwe ya Hajj au Umra

 

•     Uifanye katika muda wake unaotakiwa kisheria

 

•     Uanzie Swafā na umalizie Marwah

 

•     Ufanye Sa’iy mara baada ya kumaliza Tawāf

 

•     Uhakikishe umefanya mizunguko saba iliyokamilika ukianzia Swafā na kumalizia Marwah

 

•     Kubakia katika hali ya Ihraam wakati wa kutekeleza Sa’iy

 

Yanayopendeza wakati wa kufanya Sa’iy

 

  • Kufanya Istilaam kabla ya kuanza Sa’iy  (Ni kulibusu au kuligusa Hajar al as-wad (jiwe jeusi). Ikishindikana kufanya Istilaam unaweza kuliashiria tu kwa mkono.)

 

  • Kufanya Sa’iy mara tu baada ya kumaliza Tawāf (kusiwe na muda kati ya hizi ibada mbili)

 

  • Kuikabili Al Ka’abah kila utakapofika Swafā na Marwah

 

•     Si lazima uwe katika hali ya tohara utakapofanya Sa’iy ingawa ni vizuri zaidi na hupendeza kama utakuwa na udhu (Tofauti na Tawāf ambapo ni lazima uwe katika hali ya tohara ni mojawapo ya masharti ya kusihi Tawāf.)

 

  • Kwenda mwendo wa haraka kati ya Maylayn al-Akhdharayn – kwenye nguzo mbili za kijani kwa mwanamme

 

•     Baada ya kumaliza kunywa maji ya Zamzam, ni Sunnah kurudi tena na kulibusu Hajar al as-wad ikiwezekana au kuliashiria na kisha kuelekea sehemu ya Sa’iy ambayo imewekewa alama maalum kukuongoza.

 

•    Ukifika elekea moja kwa moja kwenye Jabal Swafāa (Lipo karibu na Al Ka’abah)

 

•    Ukifika utaweka mguu kwenye Jabal Swafāa na kisha utasoma:

 

إِنَّ ٱلصَّفَا وَٱلۡمَرۡوَةَ مِن شَعَآٮِٕرِ ٱللَّهِ‌ۖ فَمَنۡ حَجَّ ٱلۡبَيۡتَ أَوِ ٱعۡتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيۡهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا‌ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيۡرً۬ا فَإِنَّ ٱللَّهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ

 

Inna Swafāa walmarwata min sha’aairi Llaah, faman hajjal bayta awi’itamara falaa junaaha A’layhi an yatawwafa bihimaa, waman tattawa’a khayran, Fainna Llaaha Shaakirun a’liym

 

(Hakika vilima vya Swafāa na Marwah ni katika alama za Allaah. Basi anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anayejitendea mwenyewe kheri basi bila ya shaka Allaah ni Mwenye shukrani na Mjuzi).

 

•     Baada ya kumaliza kuisoma aya hii utasema:

 

•       نـــبدأ بمـــا بـــدأ الله بـــه

 

•      Nabdau bimaa bada-a Llaahu bihi (Tunaanza kwa kile ambacho Allaah alianzia).

 

•     Kisha utapanda Jabal Swafāa mpaka sehemu ambayo utaweza kuiona Al Ka’abah, hapo utaelekea Al Ka’abah kisha utasoma:

 

•الله أكبر، الله أكبر، الله أكبر

 

Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, Allaahu Akbar ,

 

•   (Allaah ni Mkubwa, Allaah ni Mkubwa, Allaah ni Mkubwa

 

•لَا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيْكَ لَهُ، لَهُ الـمُلْكُ ولَهُ الـحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ

 

•    Laa Ilaaha Illa Llaahu wahdahu Laa shariyka lahu, lahul mulk walahul hamd yuhyii wayumiitu wahuwa a’laa kulli shay in Qadiyr.

 

•   Hapana Mola isipokuwa Allaah Yuko peke yake na hana mshirika,Ufalme ni wake na Shukrani ni zake anaehuisha na anaefisha na Yeye ni Muweza wa kila jambo.

 

لا إله إلا الله وحده لا شريك له، أنجز وعده و نصر عبده وهزم الأحزاب وحده

•   Laa ilaaha illa Llaahu wahdahu Laa shariyka lahu, anjaza wa’adah, wanasara a’bdah, wahazamal ahzaaba wahdah,

 

•   Hapana Mola isipokuwa Allaah yupo peke yake, Ametekeleza miadi yake, Amemnusuru mja wake na kuyashinda makundi yote peke yake).

 

•   Ukimaliza utashuka na kuanza Sa’iy kuelekea Marwah katika njia iliyowekwa.

 

•    Unaweza kuomba duā kuleta dhikr, kujiombea mwenyewe, kuiombea familia, ndugu na jamaa pamoja na waislamu kwa ujumla. Hakuna duā maalum.

 

•   Kila ukifika kwenye alama zenye rangi ya kijani (taa rangi ya kijani zimewekwa kwa juu) wakati ukienda Marwah na ukienda Swafā utaongeza mwendo na kwenda matiti mpaka mwisho wa taa utaendelea mwendo wa kawaida

 

•   Kila ukifika na kupanda Jabal Marwah utaelekea Al Ka’abah na kuomba duā kama ulivyoomba kwenye Jabal Swafā na kisha kuendelea hadi Jabal Swafā.

 

•    Utaanzia Jabal Swafā na mzunguko wa saba utamalizia Jabal Marwah.

 

 

Baadhi ya makosa yanayofanyika wakati wa Sa’iy

 

•    Kuashiria na kusema Allaahu Akbar wakati unapopanda Jabal Swafā au Marwah.

 

•    Wanawake kwenda matiti kwenye alama za rangi ya kijani .

 

•    Kutia Udhu na kudai kwamba kila hatua utakayokwenda kwenye Sa’iy utafutiwa dhambi 70,000.

 

•    Kuongeza mwendo na kwenda mwendo wa kasi kwa sehemu yote ya Sa’iy.

 

•    Kusali Rakaa mbili baada ya kumaliza Sa’iy.

 

•    Mwanamke kutofanya Sa’iy kwa kuwa yupo katika siku zake za hedhi au nifasi.

 

•    Kuendelea kufanya Sa’iy baada ya sala ya jamaa kukimiwa.Kidokezo

 

•    Wakati unaendelea kufanya Sa’iy na kujisikia kuchoka unaweza kupumzika.

 

•    Pia unaweza kwenda msalani ila kumbuka tu idadi ya Sa’iy ulizofanya na ukirudi unaendelea tu bila ya kuanza upya.

 

•    Endapo wakati unaendelea kufanya Sa’iy imesadifu kuingia wakati wa Sala ya Fardhi na imekimiwa wakati hujakamilisha Sa’iy; utasita hapo ulipo na kuunganika na waislamu kusali jamaa na baada ya sala kukamilika utaendelea na Sa’iy bila ya kuanza upya.

 

•    Inajuzu kufanya Sa’iy ukiwa katika kipando (ingawa haipendezi ni makruhu) au kutembea kwa miguu ambayo ni bora zaidi.

Kunyoa au kupunguza nywele

 

•     Baada ya kumaliza Sa’iy ni kunyoa au kupunguza nywele.

 

•     Kunyoa ni bora zaidi kwa Mwanamme kuliko kupunguza kwani Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) aliwaombea duā ya rehma na kuwaombea maghfira mara tatu walionyoa na mara moja tu waliopunguza.

 

•     Ikiwa muda wa kuanza Hijja upo karibu mno baada ya kumaliza Umra ni vyema kupunguza nywele kwa mwanamme na utazinyoa wakati ukimaliza Hijja.

 

•      Mwanamke hatotakiwa kunyoa bali atakata nywele zake kiasi cha saizi ya pingili cha kidole.

 

Tanbihi

 

•   Haijuzu na ni haramu kwa mtu kutafuta mkasi mdogo na kujikata nywele mwenyewe kwani bado upo katika hali ya Ihraam. Tafuta mtu mwengine akufanyie.

 

•   Baada ya kumaliza mambo yote tuliyoyataja, Umra itakuwa imekamilika na utakuwa na umeshatahallal yaani umetoka katika hali ya Ihraam na kuruhusiwa kufanya yale yote ambayo uliyokatazwa ukiwa Muhrim.

Ziara ya Msikiti wa Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) Madina

 

Kufanya ziara mji wa Madina na kuzuru Msikiti wa Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) ni mojawapo ya mambo yanayofanyika wakati Muislamu anapokwenda kutekeleza ibada ya Hijja au Umra.

 

Hata hivyo Safari hii inaweza kufanywa wakati wowote mwengine na si lazima iwe ni wakati wa Hijja au Umra tu kwa sababu ziara hii si miongoni mwa matendo ya Hijja au Umra .

 

Kufanyika wakati huu ni kwa kuwepo wepesi wa kuwepo katika maeneo matakatifu.

 

Fadhila za mji wa Madina

 

•     Ni ardhi ambayo Mtume (صلى الله عليه وسلم) alifanya Hijra na kuhamia.

 

•     Watu wake ndio waliomnusuru Mtume (صلى الله عليه وسلم) na kumsaidia (Ansaar).

 

•     Ndio mji wa Iman, ni mji ambao (Iman itakapopotea) itaanzia kurudi baada ya kupotea siku za mwisho.

 

•     Kwenye Milango yake ya kuingia kuna Malaika wanaulinda.

 

•     Si Dajjaal wala maradhi yoyote ya kuambukiza yataingia Mji huu.

 

•     Utakuwa mji wa mwisho kabisa kuharibiwa.

 

•     Ni mji ambao Wahy ulikuwa ukiteremka.Kuna malipo makubwa kuzuru Msikiti wa Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) kwani amesema: Sala (moja) katika Msikiti wangu ni bora kuliko sala elfu moja kwengineko isipokuwa al Masjid al Haraam

 

 

Malengo ya kuzuru mji wa Madina

 

•      Kufanya ziara katika Msikiti wa Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) na kupata fadhila za kusali ndani yake

 

.•     Kuwepo katika sehemu ambayo ni mojawapo katika viunga vya peponi (Rawdhah).

 

•      Kupata nafasi ya kulizuru kaburi la Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ).

 

•      Kuzuru Makaburi ya Al Baqi’i na Mashahidi wa Uhud.

 

•      Kuzuru Masjid Quba.Tanbihi Muhimu

 

•      Ni Misikiti miwili tu iliyopo Madina hufanyiwa ziara kwa lengo la kufanya Ibada ndani yake: Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم) na Masjid Quba (Msikiti wa kwanza kujengwa Madina).

 

•      Misikiti mengine na maeneo mengine kama yatatembelewa ni kwa ajili ya umuhimu wake kihistoria tu na si vyenginevyo.

 

•      Si miongoni mwa wajibu za, au masharti ya, Hajj au Umra kufanya ziara Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم) au kaburi lake.

 

•      Kuna hadithi nyingi zilizozushwa kuhusu kufanya ziara kaburi la Mtume (صلى الله عليه وسلم). Kuwa na tahadhari na hadithi hizi, hakikisha kwa kuzithibitisha usahihi wake kabla ya kuzifanyia kazi.

 

Utakapofika Msikitini utaingia kwa mguu wa kulia, kisha utaomba kwa kusema:

 

أَعُوذُ بِاللَّهِ الْعَظِيمِ وَبِوَجْهِهِ الْكَرِيمِ وَسُلْطَانِهِ الْقَدِيمِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ بِسْـمِ الله، وَالصَّلاةُ وَالسَّلامُ عَلى رَسولِ الله، اللّهُـمَّ افْتَـحْ لي أَبْوابَ رَحْمَتـِك

 

Auudhu Billaahil a’dhiym wabiwajhihil kariym wasultwaanihil qadiym mina shaytwaani rrajiym, BismiLlaah, Wasswalaatu Wassalaamu a’la Rasuuli Llaah, Allaahumma ftah liy abwaaba rahamtika.

 

 

•     Na wakati wa kutoka utaomba kwa kusema:

 

BismiLlaah, Wasswalaatu Wassalaamu a’la Rasuuli Llaah, Allaahumma inniy as-aluka min fadhlika

 

•     Baada ya kuingia Msikitini Sali rakaa mbili Tahiyyatul Masjid kwa ajili ya kuamkia Msikiti.

 

•     Elekea eneo liliopo kaburi la Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) na kusimama mbele yake ikiwezekana kama hakuna msongamano na kisha kwa utulivu na unyenyekevu wa hali ya juu useme kwa ufupi tu:

 

اَلسَّلَامُ عَلَيْكَ يَا رَسُولَ اللهِ وَرَحْمَةُ اللهِ وَبَرَكَاتُهُ

 

Assalaamu a’layka Yaa Rasuulu Llaah warahmatu Llaahi wabarakaatuh

 

(Amani iwe juu yako Ewe mjumbe wa Allaah na Rehema za Allaah na Baraka zake) au

 

اَلسَّلَامُ عَلَيْكَ أَيُّهَا النَّبِيُّ وَرَحْمَةُ اللهِ وَبَرَكَاتُهُ

 

Assalaamu a’layka Ayyuhan Nabiyyu warahmatu Llaahi wabarakaatuh

 

(Amani iwe juu yako Ewe Nabii na Rehema za Allaah na Baraka zake)

 

•     Au ukitaka kwa kirefu utasoma:

 

اَلسَّلَامُ عَلَيْكَ يَا رَسُوْلَ اللهِ السَّلَامُ عَلَيْكَ يَا خَيْرَةَ اللهِ مِنْ خَلْقِهِ اَلسَّلَامُ عَلَيْكَ يَا سَيِّدَ الْمُرْسَلِيْنَ وَخَاتَمَ النَّبِيِّيْنَ

 

Assalaamu a’layka yaa Nabiyya Llaah, Assalaamu a’layka yaa khayrata Llaahi min khalqihi, Assalaamu a’layka yaa sayyidal mursaliyn, Wakhaataman Nabiyyiin

 

(Amani iwe juu yako Ewe Nabii wa Allaah, Amani iwe juu yako Ewe kiumbe bora wa Allaah, Amani iwe juu yako Ewe bwana wa Mitume na na wa mwisho katika Manabii).

 

أَشْهَدُ أَنَّكَ بَلَّغْتَ الرِّسَالَةَ وَأَدَّيْتَ الأَمَانَةَ وَنَصَحْتَ الأُمَّةَ وجاهدت في الله حق جهاده

 

Ash-hadu annaka qad balaghtar Risaalata, wa-addaytal amaanata, wanaswahtal ummata, wajaahadta fiLlaahi haqqa jihaadihi

 

(Ninashuhudia kwamba hakika umefikisha ujumbe, na umetekeleza amana, na umeunasihi Ummah na ukapigana Jihadi kwa ajili ya Allaah haki ya kupigania).

 

•     Baada ya kumsalimia Mtume (صلى الله عليه وسلم), utaelekea upande wa kulia kidogo na kisha utamsalimia Abubakr Asswiddiyq, (رضي الله عنه) kwa ufupi kwa kusema:

 

Assalaamu a’layka yaa Abaa Bakr.

 

Au kwa urefu na kusema:

 

السلام عليك يا أبا بكر الصديق ورحمة الله وبركاته , السلام عليك يا خليفة رسول الله وجزاك عن أُمّة محمدٍ خيراً

 

Assalaamu a’layka yaa Abaa bakr Asswiddiyq. Assalaamu a’layka yaa khaliyfata Rasuuli Llaah (صلى الله عليه وسلم), radhiya Llaahu a’nka, wajazaaka an ummati Muhammadin khayraa

 

(Amani iwe juu yako Ewe Abubakr Asswiddiyq. Amani iwe juu yako Ewe Khalifa wa Mtume (صلى الله عليه وسلم). Radhi za Allaah zikufikie na akulipe kutokana na Umma wa Muhammad kheri)

 

•    Baada ya kumsalimia Abu Bakr Asswiddiyq, (رضي الله عنه), utalekea tena upande wa kulia kidogo tu na kumsalimia U’mar Ibnul Khattaab, (رضي الله عنه) kwa ufupi na kusema:

 

Assalaamu a’layka yaa U’mar. Au kwa urefu na kusema:

 

السلامُ عليك يا عمر، السلام عليك يا أمير المؤمنين، رضي الله عنك، وجزاكَ عن أُمّة محمدٍ خيراً

 

Assalaamu a’layka yaa U’mar, Assalaamu a’layka yaa Amiyral Muuminiyn, radhiya Llaahu a’nka, wajazaaka an ummati Muhammadin khayraa

 

(Amani iwe juu yako Ewe U’mar. Amani iwe juu yako Ewe Kiongozi wa Waumini. Radhi za Allaah zikufikie na akulipe kutokana na Umma wa Muhammad kheri).

 

•   Baada ya kumaliza kumsalimia U’mar ibnul Khattaab (رضي الله عنه) uondoke kwani sehemu hii si sehemu ya kuomba duā kama alivyokuwa akifanya Abdullah ibn U’mar ibnul Khattaab, (رضي الله عنهما), hakuwa akiongeza jambo lolote zaidi ya kuwasalimia tu na kisha kuondoka.

 

Mambo muhimu ya kufanya ukiwa Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم)

 

1    Kuwepo Msikitini kwa muda mrefu kwa ajili ya Ibada.

 

2    Kufanya i’tikaaf.3Kuomba duā kwa wingi.

 

4    Kuomba maghfira kwa wingi.

 

5    Kusoma Qur’aan na adhkaar nyengine zilizothibiti.

 

6    Kuwahi mapema kwenda Msikitini.

 

7    Kujihimu kuwahi safu za mwanzo ikiwezekana.

 

8    Kusali Sala za Sunnah kwa wingi.

 

9    Kusikiliza darsa na mafundisho yanayotolewa Msikitini.

 

Baadhi ya makosa yanayofanyika ziara ya Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم)Madina

 

Asli katika mambo yote ya kisheria katika dini yetu ni kufanya jambo kwa kuwepo ushahidi usiokuwa na shaka kutoka katika Qur’aan au kutoka katika Sunnah za Mtume wetu (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) au kutokana na ufahamu wa Masahaba waliokuwepo enzi za Mtume (صلى الله عليه وسلم).

 

Hivyo kufanya jambo lolote kinyume na mafundisho ni makosa kama:

 

1     Kufuta kuta zilizo karibu na kaburi, Mihraab na Minbar ya Mtume (صلى الله عليه وسلم)na kuomba baraka.

 

2     Kulizunguka kaburi la Mtume (صلى الله عليه وسلم)mara kadhaa kwa ajili ya kufanya kama Tawāf.

 

3     Kumuomba Mtume (صلى الله عليه وسلم) kwa mahitaji yetu na maombi yetu.

 

4     Kulitembelea kaburi la Mtume (صلى الله عليه وسلم) kila siku.

 

5     Kusali sala 40 katika Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم).

 

6    Kwenda moja kwa moja kaburi la Mtume (صلى الله عليه وسلم) badala ya kuingia Msikitini kwanza na kusali.

 

7    Kuandika maombi na kuyadondosha kwenye kaburi la Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Fadhila za Rawdhah Annabawiyyah

 

Rawdhah Annabawiyyah ni sehemu ndogo iliyopo ndani ya Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم)ambayo ipo kati ya nyumba yake aliyokuwa akiishi na Minbar yake.

 

Sehemu hii kwa sasa imewekwa zulia maalum la kijani isiyokoza iliyochanganyika na maua ya rangi nyengine tofuati na sehemu nyengine za Msikiti.

 

Ni sehemu ndogo ambayo haiwezi kuingia watu wengi na msimu wa HIjja huwa na msongamano mkubwa.

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah, (رضي الله عنه) amesema: Mtume(صلى الله عليه وسلم) amesema:

 

Kati ya nyumba yangu na Minbar yangu kuna bustani katika bustani za peponi. Na Minbar yangu ipo katika hodhi langu.

 

Ni vizuri kusali rakaa mbili za Sunnah au sala nyengine za Sunnah kwenye Rawdhah Annabawiyah

 

Kutokana na hadithi ya Yazid bin Abi Ubayd, (رضي الله عنه), amesema:

 

Nilikuwa niko na Salamah ibn Ak Akwah (رضي الله عنه) na alikuwa akisali kwenye nguzo iliyowekwa misahafu. Nikasema Ewe Abu Muslim! Nakuona unapenda kusali kwenye nguzo hii (ni kwanini?). Akasema: Nilikuwa nikimuona Mtume (صلى الله عليه وسلم) akipenda kusali sehemu hii.

 

.

 Ziara ya Masjid Quba

 

Moja katika mambo anayotakiwa kufanya mwenye kufanya ziara ya Madina ni kuzuru Masjid Quba ambao upo nje kidogo ya mji wa Madina.

 

Ni mojawapo ya mambo aliyokuwa akifanya Mtume (صلى الله عليه وسلم) kila siku ya Jumamosi.

 

Abdullah ibn U’mar, (رضي الله عنهما), amesema:Alikuwa Mtume (صلى الله عليه وسلم) akizuru Masjid Quba kila siku ya Jumamosi (mara nyengine) kwa miguu na (mara nyengine) akiwa kwenye kipando

 

Na katika riwaya nyengine: Alikuwa Mtume (صلى الله عليه وسلم) akizuru Masjid Quba (mara nyengine) kwa miguu na (mara nyengine) akiwa kwenye kipando na kusali rakaa mbili

 

Fadhila za kuzuru Masjid Quba na kusali rakaa mbili ndani yake ni sawa na fadhila za kufanya Umra kwa mujibu wa hadithi ya Sahl bin Hanif, (رضي الله عنه) aliposema: Mtume (صلى الله عليه وسلم) amesema:

 

Mwenye kutia udhu nyumbani kwake na kuja katika Msikiti huu (akikusudia Masjid Quba) na kusali ndani yake ujira wake ni sawa na ujira wa Umra.

Ziara ya makaburi ya Al Baqi’ na mashahidi wa Uhud

 

Ni Sunnah kwa wanaume kufanya ziara kwenye makaburi ya Al baqi’i yaliyopo kando ya Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم) Madina na mashahidi wa Uhud yaliyopo katika Mlima Uhud nje kidogo ya mji wa Madina.

 

Eneo la Baqi’i ndipo walipokuwa wakizikana masahaba na mashahidi waliokufa katika vita vya Jihaad kwa ajili ya Allaah A’zza wa Jalla enzi za Mtume (صلى الله عليه وسلم) na masahaba baada yake.

 

Eneo la Uhud ndipo walipozikwa Mashahidi waliofariki katika vita vya Uhud.

 

Kutoka kwa Ummul Muuminiyna A’aishah,( رضي الله عنها), amesema:Hakika Mtume (صلى الله عليه وسلم) alikuwa akitoka usiku mkubwa (karibu na alfajiri) kwenda al Baqi’ na kuomba;

 

السَّلامُ عَلَيْكُمْ دَارَ قَوْمٍ مُؤمِنينَ، وأَتَاكُمْ مَا تُوعَدُونَ، غَدًا مُؤَجَّلُونَ، وإِنَّا إِنْ شَاءَ اللَّهُ بِكُمْ لاحِقُونَ، اللَّهُمَّ اغْفِرْ لأَهْلِ بَقِيعِ الغَرْقَدِ

 

Assalaamu a’laykum daara qaumil muuminiyna, wa – ataakum maa tuua’duun, ghadan muajjaluun, wainnaa Inshaa Allaahu bikum laahiquun, Allahumma ighfir lahlil baqii’i Al gharqad

 

(Amani iwe juu yenu nyumba ya Qaumu ya waumini, na Atakupeni aliyowaahidi, karibuni wala si mbali, na hakika sisi In shaa Allaah tutawafuatia, Ewe Mola waghufurulie ahli wa Baqi’i.)

 

Pia Mtume (صلى الله عليه وسلم) alikuwa akisoma:

 

السَّلامُ على أهلِ الدِّيارِ من المؤمنينَ والمُسْلمينَ، ويَرْحَمُ اللهُ المُستَقدِمينَ مِنَّا والمُستَأخِرينَ، وإنَّا إن شاءَ الله بكم لَلاحِقونَ

 

Assalaamu a’laa ahlid diyaari minal muuminiyna walmuslimiyna, wayarhamu Llaahul mustaqdimiyna minnaa walmusta-akhiriyna, wainnaa inshaa Llaahu bikum laahiquuna

 

(Amani kwa wenye nyumba miongoni mwa waumini na waislamu, Na Allaah Atawarehemu waliotangulia na watakaofuatia na hakika sisi In shaa Allaah tutawafuatia)

 

Ya kuzingatia wakati wa ziara ya makaburi:

 

1    Nia iwe ni kufanya ziara kwa ajili ya kutukumbusha mauti na akhera.

 

2    Kuwasalimia Masahaba na Mashahidi na kuwaombea duā tu.

 

3    Kufuata Sunnah ya Mtume (صلى الله عليه وسلم)

 

Ya kujiepusha wakati wa ziara ya makaburi:

 

1    Kuwaomba Mashahidi na Masahaba wamuombe Allaah A’zza wa Jall kwa niaba yao.

 

2    Kuwaomba msaada moja kwa moja ili ufanikiwe katika mambo yako au upate shifaa katika maradhi yanayokusumbua.

Baadhi ya maeneo na majina yanayotumika wakati wa Umra na maana zake

 

Ar Ramal: Ni ule mwendo wa kwenda kikakamavu na kuweka kifua mbele katika mizunguko mitatu ya kwanza ya Tawāf ul Quduum tu wakati wa kufanya Umra.

 

Baqi’i: Baqii’i ndipo walipokuwa wakizikana Masahaba na Mashahidi waliokufa katika vita vya Jihaad kwa ajili ya Allāh A’zza wa Jalla enzi za Mtume (صلى الله عليه وسلم) na Masahaba baada yake. Lipo pembezoni mwa Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم) Madina.

 

Bayt al A’teeq: Ni nyumba ya kale, jina jengine la Al Ka’abah

 

Dhul Hulayfah: Ni sehemu ya Miqaat kwa ajili ya kuhirimia ukitokea Madina pia sehemu hii hujulikana kama Abyar A’li.

 

Fidia: ni faini ambayo hupaswa kutolewa endapo mwenye kuhiji au kufanya Umra amefanya kosa mojawapo la kukiuka tahadhari na makatazo kwa aliyekwishahirimia.

 

Hijr: Ni ile sehemu kama nusu duara pembezoni mwa Al Ka’abah ambayo awali ilikuwa ni sehemu ya Al Ka’abah ilipojengwa na Nabii Ibraahiym A’layhis Salaam. Baada ya kujengwa tena sehemu hii ikabaki nje ya Al Ka’abah. Sehemu hii imezungushwa kwa sababu ni sehemu ya Al Ka’abah. Na haifai wakati wa kutufu kupita ndani yake.

 

Idhtibā’i: Kuivaa Ihrām na bega la upande wa kulia umeliacha wazi. Idhtiba’ai hufanyika kwenye Tawāf ul Quduum tu wakati wa kufanya ibada ya Umra.Ihlāl: Ile hali ya kuisoma talbiyah kwa sauti kubwa baada ya kuhirimia kwa Hijja au Umra.

 

Ihrām: Ni ile nia ya kukusudia kufanya ibada ya Hijja au Umra. Pia vazi analolivaa aliyekwishahirimia kwa Hijja au Umra huitwa Ihrām.

 

Ihsār: Ni vile vizuizi vinavyomzuia aliyehirimia kwa ajili ya Hijja au Umra kufanya Ibada kama ugonjwa, kuwepo vita, au mfano wake.

 

Istilām: Ni kulibusu au kuligusa Hajar al as-wad (jiwe jeusi). Ikishindikana kufanya Istilaam unaweza kuliashiria tu kwa mkono.

 

I’tikāf: Ni ile hali ya kunuia kuwepo Msikitini kwa ajili ya lengo maalum nalo ni kuwa karibu na Allāh A’zza wa Jall kwa ibada.

 

Jabal At Thawr: Ni mlima uliopo Makkah ambapo Mtume (صلى الله عليه وسلم) alijificha pamoja na Abubakr Asswiddiyq, (رضي الله عنه), wakati wakifanya Hijrah kutoka Makkah kuelekea Madina.

 

Jabal Uhud: Ni milima iliyopo nje ya mji wa Madina kiasi cha km 4 kutoka Madina. Milima hii ina urefu wa km 6 na katika sehemu hii vita vya Uhud vilipiganwa wakati wa Mtume (صلى الله عليه وسلم). Pia mashahidi waliokufa katika vita vya Uhud wamezikwa kandokando ya Milima hii.

 

Kutayammam: Ni kujitoharisha kwa kutumia mchanga kwa sababu ya kukosekana maji au kushindwa kuyatumia kutokana na udhuru fulani.

 

Kwenda matiti: Ni kwenda kwa kasi au kuongeza mwendo unapofika kwenye alama za kijani wakati ukifanya Sa’iy kwa wanaume tu.

 

Maqām Ibrāhiym: ni sehemu iliyopo ndani Msikiti wa Makkah. Asili yake ni jiwe ambalo alikuwa Nabii Ibrāhiym A’layhis Salām akisimamia wakati akijenga al Ka’abah. Sehemu hii sasa imejengewa. Allāh A’zza wa Jall Anasema: Na alipokuwa akisimama Ibrāhiym pafanyeni pawe pa kusalia

 

Manāsik: ni matendo ya Ibada ya Hiija na Umra.

 

Matāf: Ni eneo maalum ambalo Tawāf hufanyika.

 

Meelān Akh dharayn: Ni alama mbili zilizopo kwenye sehemu ya kufanya Sai’y. Sehemu hii imewekewa taa maalum za kijani na ipo karibu na jabal Swafā. Ukifika sehemu hii unatakiwa kukazana na kwenda mwendo wa kasi wakati ukifanya Sa’iy.

 

Miqaat: Ni vituo ambavyo utapaswa kuhirimia kwa ajili ya Hijja au Umra.Navyo ni Dhul Hulayfah, Qarnul Manaazil, Yalamalam, Juhfah na Dhat I’rq.

 

Multazam: ni sehemu ya Al Kaa’bah ambapo waumini huomba duā na kuomba hifadhi kutoka kwa Allāh A’zza wa Jall. Sehemu hii ipo kati ya al hajar al as-wad na mlango wa Al Kaabah

 

Sa’iy: Ni kutembea (na kwenda matiti) kati ya Jabal Swafā na Jabal Marwah. Milima miwili iliopo pembezoni mwa masjid al Harām, Makkah.

 

Tahallul: Kifunguo kinachokutoa katika hali ya kuwa katika Ihrām. Ukitahallal ina maana umeshajifungua na yale mambo yote uliyokatazwa ukiwa katika Ihrām.

 

Talbiyah: Ni dua’a ambayo hutakiwa kusomwa sana kwa kila aliyehirimia Hijja au Umra: Nayo ni Labbayka Allahumma labbayka labbayka laa shariyka laka labbayka innalhamda wanni’mata laka walmulk laa shariyka laka Dua’a hii humalizika pale utakapoingia Msikitini Masjid al haram kuanza Tawāf Umra.

 

Tamattui: Kuhirimia kufanya Hijja na Umra lakini kila moja peke yake. Hufanya Umra kwanza, unamaliza unatoka katika Ihrām kisha unahirimia tena kwa ajili ya Hijja.

 

Tani’ym: Ni sehemu iliopo nje kidogo ya Mji wa Makkah ipo kati ya Milima miwili jabal Nua’ym na jabal Naa’iym. Ndipo wakaazi wa Makkah wanapokwenda kwa ajili ya kuhirimia Umra. Pia pamejengwa Msikiti unaoitwa Masjid A’aishah.

 

Tawāf : Ni ibada ya kuizunguka al Ka’abah mara saba kwa mpigo bila ya kupumzika.

 

Tawāful Umra: Ni Tawāf ambayo hufanyika unapowasili mji wa Makkah wakati unapoanza Ibada ya Umra. Tawāf hii ndiyo inayofanywa Idhtiba’ai na Ar Raml. Ni mojawapo katika Sunnah.

 

Tawāfu Tattawwu’u: Ni Tawāf ya Sunnah kila unapoingia Masjid al Harām ni Sunnah kuuamkia kwa kufanya Tawāf badala ya kusali Tahiyyatul Masjid. Tawāf hii haina ar Raml wala idhtiba’ai.

 

Wājibāt: Ni yale mambo ambayo ni wajibu kufanywa katika Umrah nayo ni kuhirimia kwenye Miqaat, kuendelea kusimama A’rafah mpaka jua litakapotua, kupitikiwa na usiku Muzdalifah, kupitikiwa na usiku Minā siku za Tashriq, kupiga (kurembea) vijiwe jamaraat, kunyoa au kupunguza nywele, kufanya Tawāf ul Widaa (Tawāf ya kuaga) .

bottom of page